Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • w73 7/15 kur. 323-329
  • Kuwatia Wengine Moyo Wavumilie

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Kuwatia Wengine Moyo Wavumilie
  • Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1973
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • UBORA WA MPANGO MPYA KULIKO ULE WA KALE
  • TWATIWA MOYO TUUONE UBORA WA MAMBO MATAKATIFU
  • FAIDA ZA KIROHO
  • Kitabu cha Biblia Namba 58—Waebrania
    “Kila Andiko, Lenye Pumzi ya Mungu, Lafaa”
  • Mna Haja ya Uvumilivu
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1973
  • Usife Moyo Katika Shindano la Mbio la Kupata Uhai!
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1998
  • Kwa Sababu Gani Iliandikwa Vile?
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1973
Pata Habari Zaidi
Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1973
w73 7/15 kur. 323-329

Kuwatia Wengine Moyo Wavumilie

1. (a) Paulo aliwasihi ndugu zake Waebrania wafanye nini? (b) Ni vizuri kutiana moyo mtu na mwenzake mara ngapi?

ILIKUWA karibu miaka tisa mifupi tu mbele ya Yerusalemu kuharibiwa na Warumi katika mwaka wa 70 C.E. mtume Paulo alipoiandika barua yake yenye nguvu sana kwa kundi la Waebrania la Wakristo katika mji wao. Katika makala ya kwanza tuliangalia aliyoyasema katika sura za kwanza na pili za barua hiyo. Katika sura ya tatu ya barua kwa Waebrania waliogeuzwa wakawa Wakristo Paulo aliwasihi ndugu zake Waebrania wamwangalie mtume na kuhani mkuu Yesu, aliyekuwa mwaminifu kama Mwana juu ya nyumba ya Mungu. Wakristo wanayo mbele yao nafasi ya kuwa wa nyumba hiyo wakiushikilia sana uhuru wa kusema na kujivunia kwao tumaini mpaka mwisho. Hiyo maana yake ni kuvumilia. Inawapasa Wakristo waepuke kukuza “moyo mbovu wa kutokuamini, kwa kujitenga na Mungu aliye hai,” bali, inawapasa waendelee kuonyana na kutiana moyo mtu na mwenzake kila siku maadamu iitwapo “leo.”​—Ebr. 3:12, 13.

2. Katika sura ya nne ya kitabu cha Waebrania, Paulo aliwatiaje moyo ndugu zake?

2 Katika Maandiko yako maneno mengi mema ya kushauri, mifano mingi kwetu kuangalia. Paulo aliwakumbusha Wakristo Waebrania huko Yerusalemu juu ya mingine ya mifano hii ili awatie moyo. Alieleza namna Mungu alivyochukizwa na Israeli wa kale na asivyowaruhusu wengi wa Waebrania wazee waliotoka Misri waingie katika Nchi ya Ahadi. Sababu gani sivyo? Kwa maana, wakikosa imani, walitenda kwa kutokutii. Sasa, hatutaki kuikosa ahadi kwa njia ile ile. Habari njema zimetangazwa kwetu sisi, na tukitumia imani yetu tunaweza kuwa wenye uhakika wa kuingia katika ‘raha ya Mungu.’ Kwa hiyo tunaonyana mtu na mwenzake na kutiana moyo mtu na mwenzake tusije tukaangukia mfano ule ule wa kutokutii kama walivyofanya waliotoka Misri. Sikuzote imetupasa tuzione habari njema zilizotangazwa kwetu kwa ubora mwingi sana na kuzidi kuifanya imani yetu yenye nguvu. Acha Neno la Mungu litumie nguvu zake katika maisha zetu. “Maana Neno la Mungu li hai, tena lina nguvu, tena lina ukali kuliko upanga uwao wote ukatao kuwili, tena lachoma hata kuzigawanya nafsi na roho, na viungo na mafuta yaliyomo ndani yake; tena li jepesi kuyatambua mawazo na makusudi ya moyo.”​—Ebr. 4:1-5,11, 12.

3. Ni hali gani ambazo zingalikuwa mtego kwa Wakristo Waebrania?

3 Wakristo Waebrania hao wa karne ya kwanza waliishi kati ya makundi makubwa ya Wayahudi waliozoea dini ya mapokeo ya waalimu wa Kiyahudi, na waliojaribu kulifuata agano la torati ijapokuwa lilikuwa limekwisha. Wakristo walikuwa wachache na hivyo hawakupendwa na watu wengi, wakateswa na kuchukiwa. Lakini wasingeweza kuanza kuwaza juu ya kuirudia dini ya Wayahudi ili waepuke chuki na mateso, wala wasingeweza kujiacha wavutiwe kwenye furaha za sikukuu za kijamii zilizokamatana na masinagogi. Iliwapasa wawe na ujuzi wa kweli na ufahamu wa ambavyo Kristo alivyoitimiza Torati, ili waangalie wasije wakarudia nyuma kwenye dini ya Wayahudi na kutoa dhabihu za wanyama, yote ambayo sasa hayakuwa na maana yo yote, utaratibu usio na maana machoni pa Mungu.

4. Ni mafundisho gani mengine aliyoyatia Paulo katika barua yake ili awajenge Waebrania?

4 Je! chini ya hali hizi, ni nani ambaye angeweza kuufahamu zaidi kuliko mtume Paulo mkazo na mateso ambayo walipasishwa Wakristo wa Kiyahudi huko Yerusalemu? Ni nani aliyekuwa tayari zaidi kuliko Paulo, aliyekuwa Farisayo, kuwapa sababu zenye nguvu kwa kuyakanusha mapokeo ya Kiyahudi? Akiwa na ujuzi wake wa sheria ya Musa aliyojifunza miguuni pa Gamalieli, aliweza kutoa uhakika usioweza kupingwa kwamba Kristo ndiye utimizo wa Torati, pamoja na maagizo yake na dhabihu, na kwamba mpango wa kwanza sasa ulikwisha jazwa nafasi yake na mambo ya hakika yaliyo matukufu. Mafundisho yote mazuri ajabu juu ya Kristo hapa yalitolewa kwa waongofu wa Kiyahudi ukiwako uhakika mwingi kutoka katika Maandiko ya Kiebrania hivyo kwamba hakuna mtu mwenye busara angeweza kushindwa kusadikishwa na kujengwa kwa kiroho. Barua kwa Waebrania inauonyesha upendo mwingi sana wa Paulo kwa ndugu zake na tamaa yake yenye kuwaka ya kuwasaidia wao kwa njia inayofaa katika wakati wao wa haja kubwa ya kiroho.

UBORA WA MPANGO MPYA KULIKO ULE WA KALE

5. Aliukaziaje ubora wa mpango mpya wa Kikristo?

5 Uchunguzi wa barua hii kwa Waebrania unaonyesha namna Paulo alivyotilia mkazo ubora wa mpango mpya alioufanya Mungu kwa watu wake. Chini ya taratibu hii mpya ya mambo Yesu Kristo akawa kuhani mkuu milele, asiyehitaji warithi wo wote, kama walivyohitaji makuhani wakuu siku za kale za Walawi. Hana haja ya kutoa dhabihu kila siku kwa dhambi zake mwenyewe halafu kwa dhambi za watu kama walivyofanya makuhani wakuu hao. Alitoa dhabihu moja kwa dhambi za watu kwa muda wote, kisha akaketi mkono wa kuume wa Mungu.​—Ebr. 6:20; 7:11-28; 8:1; 9:6-28.

6. Kwa sababu gani agano jipya likawa bora sana kuliko agano la torati?

6 Sasa agano jipya linalofanya mambo ambayo yasingeweza kufanywa na agano la torati wakati wo wote limeanza kufanya kazi. Agano la torati lilizidi kuwakumbusha watu dhambi zao, likitaka kwamba waendelee kutoa dhabihu. Na hali, halikuweza kumfungulia mwanadamu njia ya kupata uzima wa milele. Paulo aliutaja unabii wa Yeremia juu ya agano jipya ambalo Yehova angefanya: “Hili ni agano nitakaloagana nao baada ya siku zile, anena [Yehova], nitatia sheria zangu mioyoni mwao, na katika nia zao nitaziandika.” Na akaendelea kutaja: “Dhambi zao na uasi wao sitaukumbuka tena kabisa.” “Basi, ondoleo la hayo likiwapo,” Paulo anatoa sababu, “hapana toleo tena kwa ajili ya dhambi.” (Ebr. 10:16-18; 8:7-13; Yer. 31:31-33) Kwa hiyo lililo jipya ni lenye ubora mwingi kuliko lile la kale katika njia nyingi.

7. (a) Paulo aliukaziaje ubora wa kuwa na imani? (b) Mfano wa Yesu ulionyeshaje ukamatano wa imani na uvumilivu?

7 Katika sura ya 11 ya barua ya Paulo kwa Waebrania imani ilitiliwa mkazo kama inayotakiwa sana sana, kwa kuwa pasipo hiyo haiwezekani kumpendeza Mungu. Waebrania waliogeuzwa wakawa Wakristo waliyajua mambo yaliyowapasa babu zao, wanaume waaminifu wa kale. Kwa hiyo Paulo alitumia yaliyompata Ibrahimu na wale wanaume wengine wenye imani kama njia ya kutia moyo. Wanaume hao wa Mungu wenye kujitoa walionyesha haja yenyewe ya kuendelea kuwa wenye imani yenye nguvu wakati wa majaribu mengi. Halafu katika sura ya 12 Paulo aliendeleza sababu yake kwa kuelekeza kwa Wakili Mkuu na Mkamilishaji wa imani yetu, akisema: “Basi na sisi pia, kwa kuwa tunazungukwa na wingu kubwa la mashahidi namna hii, na tuweke kando kila mzigo mzito, na dhambi ile ituzingayo kwa upesi; na tupige mbio kwa saburi katika yale mashindano yaliyowekwa mbele yetu, tukimtazama Yesu, mwenye kuanzisha na mwenye kutimiza imani yetu; ambaye kwa ajili ya furaha iliyowekwa mbele yake aliustahimili msalaba na kuidharau aibu, naye ameketi mkono wa kuume wa kiti cha enzi cha Mungu. Maana mtafakarini sana yeye aliyestahimili mapingamizi makuu namna hii ya watendao dhambi juu ya nafsi zao, msije mkachoka, mkizimia [nafsini] mwenu.” (Ebr. 12:1-3) Uvumilivu mwaminifu wa Kristo ndio mfano wetu wa kuiga. Yeye alivumilia usemi mkaidi na maumivu kwa maana kwa imani angeweza kuona, nyuma ya kifo, furaha itakayofuata. Ikiwa imani yetu ni yenye nguvu, hivyo kwamba tunaiona Taratibu Mpya iliyo mbele yetu, imetupasa hata sisi tuweze kuvumilia. Kwa kukazia hivyo ubora wa mfano wa Kristo na mpango wa Kikristo, Paulo aliweza kuwaonya watumishi wa Mungu wenzake waendelee kuona ubora mwingi wa mambo matakatifu.

TWATIWA MOYO TUUONE UBORA WA MAMBO MATAKATIFU

8. Je! utakaso na ubora wa mambo matakatifu unakamatanaje na uvumilivu?

8 Yeye alionyesha ubora wa utakaso na usafi vile vile, akivifunganisha hivi pamoja, kwa njia hii: “Tafuteni kwa bidii kuwa na amani na watu wote, na huo utakatifu, ambao hapana mtu atakayemwona Bwana asipokuwa nao; mkiangalia sana mtu asiipungukie neema ya Mungu; shina la uchungu lisije likachipuka na kuwasumbua, na watu wengi wakatiwa unajisi kwa hilo. Asiwepo mwasherati wala asiyemcha Mungu, kama Esau, aliyeuuza urithi wake wa mzaliwa wa kwanza kwa ajili ya chakula kimoja. Maana mwajua ya kuwa hata alipotaka baadaye kuirithi baraka, alikataliwa maana hakuona nafasi ya kutubu, ijapokuwa [alitafuta sana mageuzi katika nia ya baba yake] kwa machozi.” (Ebr. 12:14-17) Ndiyo, Esau hangeweza kuushika ubora wa mambo matakatifu hata katika mkazo mdogo wa kuona njaa. Hakuwa na imani iliyotakiwa ili aone furaha ambayo ingewajia walio waaminifu. Alishindwa kulivumilia jaribu dogo kama hilo. Katika hizi “siku za mwisho” upungufu wa chakula utakuwapo na sisi vile vile huenda tukaona njaa wakati fulani. Lakini hiyo siyo sababu ya kupaacha mahali petu penye baraka kama watumishi wa Mungu. Yehova atatusaidia tuyashinde majaribu yetu yote, yawe ni madogo ama makubwa. (Mt. 4:1-11) Yesu ndiye mfano wetu mkubwa kwa habari hii.

9. Ni nini mojawapo ya njia bora za kujisaidia wenyewe na wengine ili tuuone ubora wa mambo ya kiroho na haja ya kuvumilia?

9 Kama dawa kwa wale ambao huenda wakawa wavivu katika kusikia kwao na wanaotelezea kwenye kutokutenda, Paulo anapendekeza: “Na tulishike sana ungamo la tumaini letu, lisigeuke; maana yeye aliyeahidi ni mwaminifu; tukaangaliane sisi kwa sisi na kuhimizana katika upendo na kazi nzuri; wala tusiache kukusanyika pamoja, kama ilivyo desturi ya wengine; bali tuonyane; na kuzidi kufanya hivyo, kwa kadiri mwonavyo siku ile kuwa inakaribia.” (Ebr. 10:23-25) Kwa hiyo tunavutwa na ubora wa kuhudhuria mikutano na vile vile kushiriki kwa kawaida katika mikutano, ili tuendelee kuuona ubora wa mambo ya kiroho. Wale ambao wamekuwa dhaifu au wamekuwa wavivu tunaweza kuwaanzisha tena katika utendaji au kuwahimiza katika upendo na kazi nzuri kwa kuwaleta kwenye mikutano ya Kikristo. Hakuna jambo jingine ambalo linaweza kukaa mahali pa mpango kama huu wa Mungu.

10. (a) Kwa sababu gani imetupasa tutiane moyo mtu na mwenzake sasa? (b) Ni sifa gani inayomvuta mtu awasaidie ndugu zake?

10 Paulo alituambia tuwe tukitiana moyo sisi kwa sisi, na kuzidi kufanya hivyo kwa kadiri mwonavyo siku ile kuwa inakaribia. Kwa kuwa tumefikia wakati katika historia ambapo mwisho wa utawala wa Shetani unakaribia sana, inakuwa lazima kuendelea kutiana moyo mmoja na mwenzake. Ingawa wengi wa Wakristo wa kweli leo huenda hawakutoka katika taratibu ya kidini ya Kiyahudi iliyopinga na kuwatesa Wakristo wa kwanza, hata hivyo, tunazungukwa na majaribu na tu chini ya mkazo wa mateso na chuki kutoka kwa vyanzo vingine vingi. Tumetoka katika Babeli Mkuu, ambaye yungali anaonekana kufanikiwa kwa njia ya mali sehemu nyingine, lakini bila shaka hatutaki kuyarudia mazoea yake maovu. Petro alionya juu ya jambo hilo. (2 Pet. 2:21, 22) Huu ni wakati wa kuendelea kuona ubora mwingi wa mambo matakatifu tuliyojifunza. Kwa sababu ya upendo uliomo ndani ya kundi la Kikristo, wote wanatamani kuona ndugu na dada zao wakivumilia na kuendelea katika njia inayoongoza kwenye uzima wa milele. Kwa hiyo, ni wakati wa kuonyana na kutiana moyo mmoja na mwenzake. Kila mmoja wetu anaweza kukumbuka alichofanya mtume Paulo ili awatie moyo na kuwasaidia ndugu zake. Alitilia mkazo kwao ubora wa mpango huu mpya ambao Mungu amewapangia watu wake. Kwa hiyo, haipaswi iwepo nia kwa upande wetu kurudi nyuma kwenye ulimwengu na taratibu zake za kidini.

11. Twafaidikaje na mambo ya kiroho aliyoandika Paulo kwa Waebrania?

11 Vile vile twaweza kufaidika kutokana na ambayo Paulo aliwaambia Waebrania, tukijikumbusha wenyewe juu ya mpango mkubwa alioufanya Yehova kupitia kwa ukuhani wa milele, faida za agano jipya, na kuondolewa kwa dhambi milele kupitia kwa dhabihu ile moja ya Kristo. Ingawa tumeyasikia mambo haya mara nyingi, si jambo la kawaida au la vivi hivi. Ni yenye ubora mwingi sana. Kurudiwa-rudiwa kwa kweli kunajenga. Kunazo nafasi nyingi bora za kusema juu ya faida za kiroho tunazozifurahia sote kama watumishi waliojiweka wakf wa Yehova katika hizi “siku za mwisho.” Kwa kukumbushana mambo haya yote ya maana tutakuwa tukisaidiana mmoja na mwenzake tusije tukarudi nyuma polepole.

FAIDA ZA KIROHO

12. (a) Kwa sababu gani kujua namna ya kuupata uzima wa milele ni jambo la pekee sana sasa? (b) Ni mambo gani mengine walio nayo sasa watu wachache sana?

12 Ni faida gani nyingine za kiroho tunazoweza kuzungumza sisi kwa sisi kama mashahidi wa Yehova wa Kikristo? Ni nyingi sana. Tunaweza kuanza kwa kusema twajua tunavyoweza kuupata uzima; tunauona ubora wa dhabihu ya ukombozi ya Kristo. (Rum. 6:23) Wafikirie wanaozoea dini ya Wayahudi na ambao wangali wakimtazamia Masihi, ama wafikirie wapagani, wanaojua machache au wasiojua cho chote juu ya Kristo na tumaini la uzima. (1 Kor. 1:18, 23) Au, mfikirie Kristendomu, ambaye amechanganyishwa na mafundisho mengi ya uongo na filosofia na asiyeuchukua mwendo unaoongoza kwenye wokovu kwa njia ya Kristo. (Linganisha Mathayo 15:1-9.) Tofauti yake, watumishi wa Yehova wamewekwa huru na mapokeo ya Babeli Mkuu. (Yohana 8:31, 32) Hatuishi kwa woga wa kuteseka katika purgatori wala moto wa mateso. Twajua kwamba wafu wanalala. Tunalo tumaini la ajabu la ufufuo. (Yohana 5:28, 29; 1 The. 4:13-18; Ufu. 20:4-13) Hatukuvurugwa na fundisho lo lote la uongo la Utatu. Tumewekwa huru na ushirikina​—kutotegemea hirizi, mifano, sanamu, kutojikokota kwa magoti yetu kupanda pande za milima au kwenye madhabahu katika sherehe za kidini. Hatutaabiki kutokana na kutojali kwa mambo ya kiroho kwa wachungaji wa uongo katika Kristendomu wala hatuonewi na viongozi wake wa kidini. (1 Kor. 10:14; Mt. 9:36; Luka 22:25, 26; 2 Kor. 1:24) Kweli hizi ni jambo la kipekee linalofahamiwa na watu wachache sana.

13. Je! wanaomtumikia Yehova wanapataje ulinzi juu ya ibada ya mashetani?

13 Fikiria namna Yehova alivyozifungua akili za watu wake na ufahamu wazione hatari za ibada ya mashetani na yanayoonekana ndani yake, kama vile unajimu na kupiga ramli, na namna anavyotoa ulinzi juu ya mambo haya. (Kum. 18:10-12; 1 Kor. 10:21; Gal. 5:19, 20; 1 Tim. 4:1; Ufu. 18:4, 23) Ingawa wengine wanaogopa, haitupasi sisi tuuogope uchawi.​—Hes. 23:21, 23; Mit. 18:10.

14, 15. Katika historia ya ulimwengu wakati huu, ni faida gani nyingine walizo nazo watumishi wa Mungu?

14 Hali za ulimwengu zinazidi kuwa mbaya siku kwa siku. Watu wanavunjika mioyo kwa woga wa yanayokuja. Kati ya watu wote mashahidi wa Yehova wa Kikristo peke yao ndio wenye tumaini la kweli kwa wakati ujao. Wakristo hawa wanao ndugu wenye upendo wanaowafariji na kuwajenga; mtu anapokuwa na uhitaji, wengine wanakuwa tayari kumsaidia. Zaidi Babeli Mkuu atakapoharibiwa kati ya mshindo mkubwa huo utakuwa wakati kwa hawa Wakristo waaminifu kufarijiana na kusaidiana mmoja na mwenzake na kuuona wokovu wa Yehova. Zitakuwako baraka nyingi kweli kweli kwa kuwa katika safu za watu wa Yehova wakati huo.​—Luka 21:26; 1 The. 5:12-15; Ufu. 17:15-18; 19:1.

15 Tunajua sababu ya uovu kuruhusiwa. Tunaifahamu maana ya “siku za mwisho” na haitupasi tuingilie siasa za ulimwengu na mchafuko. Wakristo wa kweli hawajitii katika fujo za migomo, ghasia, fitina juu ya serikali na uasi wa hizi “siku za mwisho.” Huu wote ni ulinzi kwetu.​—Kut. 9:15, 16; Ayubu 1:6–2:10; Yohana 6:15; 17:16; Rum. 13:1-9.

16. Ni mambo gani mengine tunayofaidika kwayo kwa kipekee kwa sababu ya kulijua na kuishi kwa Neno la Mungu?

16 Mashahidi wa Yehova wana faida nyingi za kipekee. Kwa kuwa hatuna mashaka ya wasio na tumaini walio katika hii taratibu ya kale ya mambo, twaweza kuepuka misiba mingi. Wasiwasi ni mojawapo ya sababu nyingi kubwa za ugonjwa wa moyo. Kwa kuzifuata sheria za Yehova zinazopasa adili tunayaepuka magonjwa ya kisonono na kaswende ya ulimwengu huu, yanayoenea kwa kasi sana katika hizi “siku za mwisho.” Tunajiepusha na tabia ya kutumia tumbako, na huu ni ulinzi wa kujikinga na donda baya sana, linalowasumbua watu wengi sana sasa. Hatuwi walevi na hivyo hatusumbuliwi na matokeo yenye kuharibu ya pombe katika akili na mwili. Hatupatwi na huzuni inayoletwa na kupata hasara michezoni ya kamari. Sikukuu za kilimwengu zinawafanya watu wengi wawe na madeni kwa kuonyesha “roho ya sikukuu,” na nyuma ya hapo wanajaribu kuyamaliza madeni haya kwa muda wa miezi mingi sana sana. Tofauti yake, ujuzi wa kweli kutoka kwa Neno la Mungu unatufanya wenye furaha, na inasemekana kwamba moyo wenye furaha ni dawa nzuri. Vile vile kunayo furaha nyingi katika kuwapa wengine kweli. Kwa hiyo kunazo baraka nyingi, katika kila njia!​—Flp. 4:6, 7; Gal. 5:19-23; Mit. 4:20-22; Mt. 5:3-12; Matendo 20:35.

17. Kwa kuzishika sheria za Mungu, ni faida gani zinazozijia jamaa za Kikristo?

17 Jamaa nyingi sana za kilimwengu zimetengana kwa kushindwa kuziheshimu sheria za Yehova. Lakini kufundisha kwa Yehova kumetusaidia sisi tuupate umoja wa jamaa. Kwa kuyafuata Maandiko, watoto waliofundishwa sawasawa na wazazi wao katika matendo ya Kikristo wanalindwa na matokeo yenye kudhuru ya uasi na dawa za kutia usingizi zinazoenea sana leo na zinazoleta wasiwasi mwingi na huzuni.​—Efe. 6:1-4; Mit. 3:1, 2.

18. Kwa maandiko, onyesha ubora wa urafiki wa Kikristo kuliko urafiki wa kilimwengu.

18 Ushirika wetu pamoja katika kundi la Kikristo na urafiki na ndugu zetu ni baraka kubwa, kwa kuwa ni furaha kweli kuwa karibu na wale wanaotokeza tunda la roho. Hivyo, hatujitii katika kazi za mwili, zenye kudhuru,​—Mit. 17:17; Gal. 5:22-26; 1 Kor. 15:33.

19. (a) Je! unaweza kufikiria sababu zaidi za kumshukuru Yehova? Nyingine ni gani? (b) Twawezaje kuvumilia mpaka mwisho?

19 Ingewezekana kuendelea na kutumia saa nyingi tukijikumbusha baraka zinazotolewa na mpango wa Yehova kwa watumishi wake. Ni akina nani wengine isipokuwa watumishi wa Yehova wanaoweza kuona maana ya ufalme wa Mungu tangu Mfalme Yesu Kristo alipoanza kutawala katika mbingu katika mwaka wa 1914 C.E.? (Zab. 2:4-6; 110:1, 4; Dan. 2:44; 7:13, 14; Mt. 11:25-27; 13:44; Ufu. 11:15-17; 19:11-21) Ni akina nani wengine wanaofahamu namna, Yehova atakavyoifanya dunia hii kuwa paradiso ambamo mwanadamu ataishi milele chini ya utawala huo wa Ufalme? (Ufu. 21:1-5; Zab. 37:9-11, 29; Mhu. 1:4; Isa. 65:17-23; Eze. 34:25-27; Luka 23:42, 43) Unapolisoma Neno la Mungu, endelea kufikiria namna Yehova alivyotupa tunayohitaji katika njia zote, na usishindwe kamwe kumshukuru Yehova. (Rum. 8:28) Ni kuona ubora wa namna hii wa mambo mazuri ya Yehova na kuwaza huku juu ya baraka zake nyingi kunakojenga na kutia moyo. Hayo ndiyo mambo ya kuzungumzwa nasi. (Matendo 14:21, 22; 1 Kor. 14:3) Hivi ndivyo tunavyoweza kusaidiana mmoja na mwenzake kukaa katika hali yetu ya kiroho. Ijapokuwa majaribu yanaweza kuja, tumepewa mipango mingi sana na Yehova kutusaidia tuvumilie. (Yak. 1:12) Kama mtu mmoja mmoja na kama makundi tumeiimarisha imani yetu kwa hiyo tuko katika hali bora ya kuvumilia mpaka mwisho, tunapoyashinda majaribu na mavutano maovu ya hizi “siku za mwisho” na kushiriki katika kutangazwa kwa habari njema. Kwa hiyo kusudi letu na liwe kama lile lililosemwa na mtume Paulo: “Basi sisi si aina ya warudio nyuma kwenye uharibifu, bali aina ya walio na imani kuhifadhi hai nafsi.”​—Ebr. 10:39, NW.

​—Kutoka The Watchtower, January 15, 1973.

[Picha katika ukurasa wa 326]

Kwa kutoa maelezo katika mikutano tunatiana moyo na kuonyana sisi kwa sisi ili tuvumilie

[Picha katika ukurasa wa 327]

Je! mambo tunayozungumza ndiyo mambo yanayoleta faida za kiroho kwa kweli?

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2026)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2026 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki