Maswali Kutoka kwa Wasomaji
● Nyama inapokatwa ikitayarishwa kupikwa, au nyuma ya kuikatakata ikiisha kupikwa, majimaji mekundu huenda yakatiririka. Je! nyama kama hiyo inafaa kuliwa na Mkristo?—U.S.A.
Mkristo anaweza kula nyama ya wanyama walioondolewa damu yao tu wakati wa kuchinjwa. Biblia inaamuru: “Mjiepushe . . . na damu, na nyama zilizosongolewa.”—Matendo 15:29.
Kweli, hata nyama ya wanyama walioondolewa damu vizuri huenda ikaonekana nyekundu sana au huenda ikawa na majimaji mekundu juu yake. Hii ni kwa sababu kuondoa damu hakuondoi kila alama ya damu katika mnyama. Lakini sheria ya Mungu haitaki kwamba kila tone moja la damu liondolewe. Inataja tu kwamba mnyama anapaswa kuondolewa damu.
Ndipo, vile vile, kuna majimaji katika nyama ambayo yakichangamana na alama zilizobaki za damu yanakuwa mekundu. Majimaji hayo yaliyo katikati ya chembe yanafanana na yale ya damu. Lakini siyo damu na kwa hivyo hayatiwi katika katazo la damu. Hivyo kuwako kwa majimaji mekundu tu hakufanyi nyama isifae kwa chakula. Mradi tu mnyama ameondolewa damu vizuri, nyama yake inaweza kutumiwa kama chakula kulingana na Maandiko.
Huenda zikawako nyakati, hata hivyo, ambazo Mkristo ana sababu ya kuamini kwamba mnyama labda hakuondolewa damu kwa kufaa. Ikiwa hana njia ya kupata uhakika, anaweza kuchagua kutoila nyama na hivyo aepuke kusumbua dhamiri yake. Hii ni kupatana na kanuni inayotajwa katika Warumi 14:23: “Aliye na shaka, kama akila, amehukumiwa kuwa ana hatia.”