Maswali Kutoka kwa Wasomaji
● Mkristo aliye wakf imempasa kulingana na Maandiko aoneje vyama vya wafanya kazi na kushiriki katika shughuli zao?
Maandiko yanawashauri Wakristo ‘waangalie yaliyo mema machoni pa watu wote.’ “Lakini mtu ye yote asiyewatunza walio wake, yaani, wale wa nyumbani mwake hasa, ameikana Imani, tena ni mbaya kuliko mtu asiyeamini.” Maandiko haya yanahusu mambo ya vyama vya wafanya kazi, kwa sababu ili kuyatii huenda ikawa lazima kujiunga na chama cha wafanya kazi. Labda ulinganifu utafanywa kati ya wajibu wa mtu kama mwanachama wa chama cha wafanya kazi na ule alio nao kama raia wa nchi. Mkristo analipa kodi kwa sababu ya faida anazopokea kutoka kwa serikali; vile vile, kwa kufaa angeweza kulipa ada za chama, kwa kuwa hiyo kweli ingekuwa bima ya kazi. Kwa hiyo, hakuwezi kuwako katazo kwa Mkristo kuwa mwanachama wa chama cha wafanya kazi tu, akilipa ada na kutii mwito wa kutofanya kazi ukitukia mgomo.—Rum. 12:17; 1 Tim. 5:8.
Walakini, isingemfaa Mkristo kujiingiza katika shughuli ya chama cha kazi kwa kadiri ya kuwa na cheo katika chama hicho. Wala, ukitukia mgomo wa kazi, isingefaa kwake kushiriki katika kuwashawishi wengine wagome au katika njia nyingine kuchochea mgomo wa kazi. Zaidi ya yote, haimpasi ashiriki katika mabishano yenye jeuri ya vyama vya kazi, kwa maana “haimpasi mtumwa wa Bwana kuwa mgomvi; bali kuwa mwanana kwa watu wote.” “Kama yamkini, kwa upande wenu, mkae katika amani na watu wote.” Kama vile Mkristo anavyokataa kuwamo katika mambo ya siasa na vita vya nchi ya kwake, vivyo mwanachama wa chama cha wafanya kazi ambaye ni Mkristo hajiingizi katika shughuli za kuongoza na katika kupigania uchumi kunakofanywa na chama cha wafanya kazi bali yeye anakataa kushiriki katika mambo haya.—2 Tim. 2:24; Rum. 12:18.